
Tanzania inasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa 2-1, baada ya
Jumatano kushinda 2-0 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa
kwanza wa hatua ya kwanza ya mchujo.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa wa Angola, Martins de
Carlvalho aliyesaidiwa na Gadzikwa Bongani wa Zimbabwe na Valdmiro
Ntyamba wa Angola, hadi mapumziko Malawi walikuwa mbele kwa bao hilo
1-0, lilifungwa na John Banda dakika ya 42 aliyefumua shuti kali
akimalizia pasi ya Chiukepo Msowoya.
Taifa Stars ndio walioanza mchezo huo kwa kasi na dakika ya
kwanza tu, mshambuliaji Mbwana Samatta alikaribia kufunga, baada ya
kumtoka beki Limbikani Mnzava, lakini kipa Simplex Nthala akaokoa.
Malawi wakajibu shambulizi dakika ya pili baada ya shuti kali la
Banda kupanguliwa na kipa Ally Mustafa ‘Barthez’. Barthez akafanya kazi
nzuri tena dakika ya 10 baada ya kuokoa michomo miwili mfululizo ya
Malawi.
Stars ilizinduka dakika ya 35 baada ya Thomas Ulimwengu kumtoka
vizuri beki wa Malawi Yamikani Fodya baada ya pasi ndefu ya Samatta,
lakini shuti lake likaenda nje sentimita chache.
Kipindi cha pili, kocha wa Stars, Charles Boniface Mkwasa
alianza na mabadiliko, akimtoa kiungo Said Ndemla na kumuingiza
mshambuliaji John Bocco.
Mabadiliko hayo yaliifanya Stars ianze kudumu kwenye eneo la
Malawi, lakini bado mashambulizi ya hatari yalielekezwa langoni mwa
Tanzania.
Dakika ya 58 Nahodha wa Tanzania, Nadir Haroub ‘Cannavaro’
aliokoa hatari langoni mwake na dakika ya 62 Malawi walifanya
mashambulizi matatu mfululizo ya hatari lanoni mwa Stars, ikiwemo kupata
kona mbili.
Dakika ya 72 Mbwana Samatta alipiga shuti hafifu akiwa karibu na lango baada ya kupokea pasi nzuri ya John Bocco likaenda nje.
Malawi walifanya shambulizi la hatari dakika ya 90, lakini Robin Ngalande akashindwa kumalizia vizuri baada ya kupiga nje.
Kwa matokeo hayo, Taifa Stars sasa itamenyana na Algeria katika mechi za mwisho za mchujo mwezi Novemba.
Kikosi cha Tanzania; Ally Mustafa ‘Barthez’, Shomary Kapombe,
Mwinyi Hajji, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kevin Yondan, Himid Mao, Thomas
Ulimwengu, Said Ndemla/John Bocco dk46, Mudathir Yahya, Mbwana Samatta
na Farid Mussa/Mrisho Ngassa dk75.
Malawi; Simplex Nthala, Stanley Sanudi, Miracle Gabeya/Robin
Ngalande dk76, Yamkani Fadya, Limbikani Mzava, Gerald Phiri, Chimango
Kayira, Micium Mhone, Chiukepo Msowoya, John Banda na Shumaker Kuwali.
No comments:
Post a Comment